Thursday, August 9, 2012

MUUMINI NA MUISLAMU


Kwanza ni vyema ifahamike kuwa maneno mawili haya: "Islaam" na "Iimaan" yana maana yao ya kilugha iliyotangulia kuwapo kabla ya kuja kwa Sharia ya Dini na yana maana ya kiistilahi iliyoletwa baadae na Sharia ya Dini.

"Islaam" kilugha ni kusalimu amri, kunyenyekea na utiifu.
"Iimaan" kilugha ni kusadiki na kuamini moyoni.

Katika istilahi ya Sharia ya Dini, kila moja kati ya maneno mawili haya limejumuisha peke yake maana hizo zote mbili za kilugha zikachanganywa kuwa maana moja maalumu ya kiistilahi iliyoletwa na Dini.
"Islaam" kiistilahi ndiyo Dini ya Allah - Uislamu. Allah S.W. anasema:

)إِنَّ الدِّينَ عِنْدَ اللَّهِ الْأِسْلامُ)

“Bila shaka dini (ya haki) mbele ya Allah ni Uislamu” (Aali Imran: 19)

Na Dini ya Allah imekusanya kumuamini Allah na nguzo zote za imani pamoja na uyenyekevu na utiifu kwa Allah kwa kutekeleza amri zake na kuacha makatazo Yake.

Kwa maneno mengine, “Iimaan” ya Dini ni ukweli uliomo ndani ya nafsi, na “Islaam” ni sura yake inayodhihiri kwa nje. Kwa hiyo mtu hawi Muislamu asipokuwa na imani; vilevile hawi Muumini asipotekeleza nguzo za Uislamu.
Kwa ajili hiyo "Islaam" na "Iimaan" katika Istilahi ya kidini hutumika kama visawe [synonyms], yaani maneno yaliyo sawa kimaana.

Hata hivyo, katika maandiko ya Sharia ya Dini, maneno haya mawili yametumika baadhi ya mwahala yakiwa tafauti na baadhi ya mwahala kwa maana moja. Yalimotumika yakiwa tofauti zimezingatiwa maana zao za kilugha, na yalimotumika kwa maana moja imezingatiwa maana yao ya kiistilahi ya kisharia ambayo inayajumuisha.

Mifano ya mwahala yalimotumika kwa maana tafauti kwa kuzingatia maana zao za asli kilugha:
1) Hadithi ya Jibril A.S. alipokuja kwa Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie- akamwambia:

(يا محمد ما الإيمان؟ قال: أن تؤمن باللّه وملائكته وكتبه ورسله واليوم الآخر والقدر خيره وشره، قال فما الاسلام، قال شهادة أن لا إله إلا اللّه وأن محمدا رسوله، وإقام الصلاة، وإيتاء الزكاة وحج البيت، وصوم رمضان. قال: فما الإحسان؟ قال: أن تعبد اللّه كأنك تراه، فان لم تكن تراه فانه يراك)

“Ewe Muhammad! Nini imani?” Mtume akasema: ‘Kumuamini Allah na Malaika Wake na vitabu Vyake na mitume Yake na Siku ya Mwisho na qadar ya kheri na ya shari.’ Akamwambia “Na nini Uislamu?” Akasema ‘Kushuhudia kuwa hakuna anayestahiki kuabudiwa ila Allah na kwamba Muhammad ni Mtume Wake, na kusimamisha sala, na kutoa zakaa, na kuhiji, na kufunga Ramadhani.’ Akamwambia “Na nini ihsani?” Akasema ‘Kumuabudu Allah kama kwamba unamuona; kwani ukiwa humuoni basi yeye anakuona.’ Imepokewa na Tirmidhi.

2) Kauli ya Allah kuhusu Mabedui walipomwambia Mtume “Tumeamini”:

( قُلْ لَمْ تُؤْمِنُوا وَلَكِنْ قُولُوا أَسْلَمْنَا وَلَمَّا يَدْخُلِ الْأِيمَانُ فِي قُلُوبِكُمْ )

[Sema: Hamjaamini, lakini semeni: Tumesilimu. Kwani Imani haijaingia katika nyoyo zenu] (Al-Hujurat: 14)

Mifano ya mwahala yalimotumika kwa maana moja ya kiistilahi (kisharia):
1) Kauli ya Allah akihadithia maneno ya Malaika waliotumwa kuwaangamiza watu wa Nabii Luut:

( فَأَخْرَجْنَا مَنْ كَانَ فِيهَا مِنَ الْمُؤْمِنِينَ . فَمَا وَجَدْنَا فِيهَا غَيْرَ بَيْتٍ مِنَ الْمُسْلِمِينَ )

[Kwa hivyo tutawatoa katika hao wale walio amini. Lakini hatukupata humo ila nyumba moja tu yenye Waislamu!] (A’Dhaariaat: 35-36)

Nyumba inayokusudiwa ni ya Nabii Luut, kaitwa yeye na binti zake “walioamini” kisha wakaitwa "Waislamu".

2) Kauli Yake S.W.:

)وَقَالَ مُوسَى يَا قَوْمِ إِنْ كُنْتُمْ آمَنْتُمْ بِاللَّهِ فَعَلَيْهِ تَوَكَّلُوا إِنْ كُنْتُمْ مُسْلِمِينَ)

[Na Musa alisema: Enyi watu wangu! Ikiwa nyinyi mmemuamini Mwenyezi Mungu, basi mtegemeeni Yeye, ikiwa nyinyi ni Waislamu] (Yunus: 84)

3) Nguzo za Uislamu kuitwa imani katika kauli ya Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie aliposema:

(أتدرون ما الإيمان بالله وحده). قالوا: الله ورسوله أعلم، قال: (شهادة أن لا إله إلا الله وأن محمدا رسول الله، وإقام الصلاة، وإيتاء الزكاة، وصيام رمضان، وأن تعطوا من المغنم الخمس).

“Je mnajua nini kumuamini Allah peke Yake?” Wakasema: Allah na Mtume Wake wanajua zaidi. Akasema: “Ni kushuhudia kuwa hakuna anayestahiki kuabudiwa ila Allah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allah, na kusimamisha sala, na kutoa zakaa, na kuhiji, na kufunga Ramadhani, na kutoa khumus ya ghanima” Imepokewa na Bukhari na Muslim.

4) Amali njema, zikiwemo nguzo za Uislamu kufanywa sharti ya mtu kuwa Muumini, kama katika kauli Yake S.W.:

)إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَاناً وَعَلَى رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ)

[Hakika Waumini ni wale ambao anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa khofu, na wanapo somewa Aya zake huwazidisha Imani, na wakamtegemea Mola wao]

)الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنْفِقُونَ)

[Hao ambao wanashika Sala na wanatoa katika yale tunayo waruzuku]

)أُولَئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقّاً لَهُمْ دَرَجَاتٌ عِنْدَ رَبِّهِمْ وَمَغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ)

[Hao kweli ndio Waumini. Wao wana vyeo, na maghfira, na riziki bora, kwa Mola wao] (Al-Anfaal: 2-4)

Vile vile kauli Yake S.W.:

)قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ)

[HAKIKA wamefanikiwa Waumini]

)الَّذِينَ هُمْ فِي صَلاتِهِمْ خَاشِعُونَ)

[Ambao ni wanyenyekevu katika Sala zao]

)وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ)

[Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi]

)وَالَّذِينَ هُمْ لِلزَّكَاةِ فَاعِلُونَ)

[Na ambao wanatoa Zaka]

)وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ)

[ Na ambao wanazilinda tupu zao]

)إِلَّا عَلَى أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ)

[Isipo kuwa kwa wake zao au kwa iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa]

)فَمَنِ ابْتَغَى وَرَاءَ ذَلِكَ فَأُولَئِكَ هُمُ الْعَادُونَ)

[Lakini anaye taka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka]

)وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ)

[Na ambao wanazitimiza amana zao na ahadi zao]

)وَالَّذِينَ هُمْ عَلَى صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ)

[Na ambao Sala zao wanazihifadhi]

)أُولَئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ)

[Hao ndio warithi]

)الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ)

[Ambao watairithi Pepo ya Firdausi, wadumu humo]
(Al-Mu’minuun: 1-11)

5) Amali njema kuitwa imani katika kauli ya Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie:

"الإِيمان بضعٌ وسبعون، أفضلها قول لا إله إلا اللّه، وأدناها إماطة العظم عن الطريق، والحياء شعبةٌ من الإِيمان"

“Imani ni matawi sabini na kitu, bora yao ni kusema ‘La ilaaha illa ’Llaah’, na ya chini yao ni kuliondoa fupa njiani; na hayaa (staha) ni tawi moja la imani.” Imepokewa na Tirmidhi, Abu Daud, Nasai na wengine.

Hivyo katika Istilahi ya Kisharia Muislamu ndiyo Muumini, na Muumini ndiyo Muislamu, hakuna tafauti baina yao.

No comments:

Post a Comment